
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro ameruhusu kusafirisha jumla ya kontena 93 ya gundi ( utomvu) ambayo sawa na tani 1,683 iliyokuwa tayari imeshavunwa wakati akitoa tamko la kuzuia usafirishaji wa malighafi hiyo kwenda nchi za nje.
Ametoa kauli hiyo leo Jijini Arusha mara baada ya kupokea ushauri kutoka kwa Kamati ya Kumshauri Waziri kuhusu masuala ya misitu kabla ya kufanya mkutano wa Wadau wa mazao ya misitu kuwa gundi hiyo ambayo imekwisha vunwa inapozidi kukaa inapoteza ubora wake na hivyo kutokufaa tena kwa matumizi tena.
Dkt.Ndumbaro amesema amelazimika kuruhusu kusafirishwa kwa tani hizo ili gundi hiyo isiweze kuharibika pamoja na kuepusha hasara ambayo ingewapata kwa wamiliki pamoja na serikali kukosa mapato kwani Serikali inapata mapato pindi malighafi hiyo inaposafirishwa.
Hatua hiyo inakuja kufuatia agizo la kusitishwa kuvunwa na kusafirishwa kwa malighafi hiyo kwenda nchi za nje alilolitoa Dkt. Ndumbaro mwezi Oktoba akiwa mkoani Iringa mara baada ya kushindwa kupata maelezo ya kutosha kuhusiana na biashara ya bei ya gundi hiyo pamoja na matumizi yake huko inakosafirishwa nchi za nje hususani China.
Katika hatua nyingine, Dkt.Ndumbaro ameendelea kushikilia msimamo wake wa kusitisha zoezi la kuvuna utomvu huo hadi pale Chuo cha Kilimo cha Sokoine ( SUA) pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania ( TAFORI) zitakapotoa utafiti wake ambao kwa sasa bado haujakamilika juu ya athari ya miti inayovunwa gundi hiyo.
