
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa ameliagiza Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kushirikiana na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuhakikisha wanaiwekea mazingira wezeshi timu ya Taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 20 Tanzanite yatakayowajenga kimwili na kisaikolojia wachezaji hao katika kuikabili timu ya taifa ya Ethiopia Januari 2022.
Waziri Bashungwa ametoa agizo hilo alipokutana nao na kufanya mazungumzo na wachezaji pamoja na kamati ya ufundi ya timu hiyo kujadili na kufanya tathimini ya changamoto mbalimbali za kimichezo zilizojitokeza wakiwa nchini Burundi wakati wa mchezo baina ya Tanzanite na wenzao wa timu ya wanawake ya Burundi ya chini ya umri wa miaka 20.
Waziri Bashungwa amesema kazi ya Serikali katika sekta ya michezo ni kuweka mazingira wezeshi kwa wanamichezo na timu zote zinazoipeperusha bendera ya taifa, na ndoto ya Serikali ni kuwaona wachezaji na timu zao wakiibuka washindi katika michezo yote.
