Back to top

VIJIJI 5 NA VITONGOJI 47 KUONDOLEWA ENEO LA HIFADHI USANGU

26 October 2022
Share

Serikali imeamuru vijiji vitano na vitongoji 47 katika vijiji 14 pamoja na sehemu ndogo ya kitongoji cha Magwalisi kilichopo mamlaka ya mji mdogo wa Rujewa Wilaya ya Mbarali kuhamishwa ili kupisha hifadhi.

Pia vitongoji 3 katika kijiji cha Lualaje wilayani Chunya navyo vinatakiwa kuondoka kupisha hifadhi.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula katika mkutano wa hadhara na wananchi wa eneo la Ubaruku Mbarali wakati Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta walipofanya ziara kwenye eneo la mto Ruaha na mnazi katika Kijiji cha Mwanavala ambapo eneo lote liko katika hifadhi.

Uamuzi huo wa serikali unalenga kutunza na kulinda ardhi oevu pamoja na vyanzo vya kupokea na kutunza maji yanayotiririka kutoka mito mbalimbali.

Bonde la Usangu ni ardhi oevu ya Usangu ni kitovu cha kupokea na kutunza maji yanayotiririka kutoka mito mbalimbali inayochangia maji kwenye mto Ruaha. 

Pia ni makazi ya Bioanuwai mbalimbali ikiwemo wanyamapori, ndege wakubwa kwa wadogo aina zaidi ya 300 , samaki na mimea ya aina mbalimbali.