Back to top

Samatta rasmi Aston Villa, asaini mkataba wa miaka 4 na nusu

21 January 2020
Share

Klabu ya  Aston Villa imemsajili nahodha wa Taifa Stars Mbwana Samatta kwa mkataba wa miaka 4 na nusu akitokea klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji.

"Nimefurahi sana," Samatta alisema. "Ni hatua kubwa kwangu katika kazi yangu. Ni hatua kubwa kwa nchi yangu pia. Kila mtu alikuwa akitafuta Mtanzania kucheza kwenye Ligi Kuu za kimataifa hatimaye nimewatoa kimasomaso.

"Ninajua mengi juu ya Aston Villa. Nilikuwa nikitazama rekodi ya Ligi kuu wakati Gabby Agbonlahor alipokuwa hapa."

Mbwana Samatta amefunga mabao 10 kwa timu yake ya awali ya Genk katika mashindano yote msimu huu ikiwa ni pamoja na bao alilolifunga huko Anfield dhidi ya Liverpool kwenye Ligi ya Mabingwa.

Meneja wa villa Dean Smith alionesha furaha yake baada ya saini kuwekwa ."Nimefurahiya sana tumefanikiwa kumleta Mbwana Samatta klabuni,"

"Amefunga mabao katika kipindi chote cha kazi yake na ninatarajia kufanya kazi naye."

Samatta atakuwa Mtanzania wa kwanza kucheza kwenye Ligi Kuu lakini hataweza kushiriki kwenye mechi ya nyumbani ya Villa dhidi ya Watford Jumanne.

Villa wamecheza mechi zao tatu za mwisho bila mshambuliaji anayetambuliwa baada ya kumpoteza mchezeshaji wa mbele mwenye asili ya Brazil Wesley kwa msimu wote baada ya kupata jeraha la goti lililodumu huko Burnley Siku ya Mwaka Mpya.