Back to top

'Yawa' yampaisha Baba Kuboye kimataifa.

01 September 2021
Share

Mkali wa Afrobeat kutoka Nigeria mwenye makazi yake nchini Marekani, Babatunmida Kuboye a.k.a Baba Kuboye ameachia kitu kipya "Yawa", wimbo ambao tayari umemuweka pazuri kimataifa.

Staa huyo mbali na kuonyesha ufundi mkubwa katika uimbaji, pia amechanganya na kionjo cha ala ya saxophone (maarufu kama Mdomo wa Bata), ala ambayo yeye ni fundi kuliko ‘fundi Maiko’.

Katika kibao hicho ambacho ametunga mwenyewe na kutayarishwa na Lebo ya Spiritual Vibes, Baba Kuboye anaonyesha ufahamu wake katika jamii mbalimbali alizoishi ikiwemo Nigeria, Uingereza na sasa Marekani ambapo anaishi na kufanya shughuli zake za muziki.

Akizungumzia kibao hicho, Baba Kuboye anasema: “Nimetoka kwenye familia ya muziki. Wazazi wangu walikuwa wanamuziki wakubwa wa Afro Jazz, ambao ndiyo waanzishi wa muziki huo nchini Nigeria. 

“Lakini pia mjomba wangu, Fela Kuti na binamu yangu, Femi Kuti na Seun Kuti walizunguka kila mahali kuonyesha namna muziki asili wa Afrobeat unavyopigwa. Naamini utaufurahia wimbo huu, kama ambavyo mimi ulinifurahisha wakati nikiutunga.”

Ujio huu wa Baba Kuboye ni mwanzo mpya wa kutengeneza mawimbi katika muziki ambao umeacha alama kubwa ya wazazi wake na familia katika kipindi cha miongo minne iliyopita.

Yeye ni mtoto wa wakongwe kwenye muziki wa Jazz: Fran na Tunde Kuboye na mjukuu wa Lejendari  wa muziki huo, marehemu Fela Kuti.