Back to top

Kabudi amkabidhi ofisi Waziri wa Mambo ya Nje Balozi Liberata Mulamula

15 April 2021
Share

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amekabidhiwa rasmi Ofisi na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo Prof. Palamagamba John Kabudi ambapo diplomasia ya siasa ya kimkakati ikiwemo diplomasia ya uchumi vikitajwa kama kipaumbele, Aprili 14, 2021.
.
Akizungumza wakati akikabidhi nyaraka na Ilani ya Chama Cha mapinduzi kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula, aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo Prof. Palamagamba John Kabudi amesema majukumu na muongozo wa utendaji kazi wa Wizara umetajwa katika ilani ya chama ikiwa ni pamoja na kuifanya sauti ya Tanzania kusikika katika medani za kimataifa sanjari na kuijenga haiba na taswira ya Tanzania katika jumuiya za kimataifa.
.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amemshukuru mtangulizi wake huyo kwa kipindi chote cha miaka miwili alichohudumu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kuweka misingi imara ya mahusiano na mataifa mengine duniani ikiwa ni pamoja na kusimamia kikamilifu mikataba yenye tija kwa Taifa na makampuni au mataifa mengine.