Back to top

 CHANJO DHIDI YA MATENDE NA MABUSHA KUTOLEWA KINONDONI 

13 November 2023
Share

Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTD), kwa kushirikiana na wadau wa Research Triangle Institute (RTI), inatarajia kufanya zoezi la umezeshaji kinga tiba, dhidi ya  Ugonjwa wa Matende na Mabusha au Ngirimaji.

Zoezi hilo linatarajia kuanzia Tarehe 6 mpaka 12 mwezi Disemba mwaka 2023, katika Manispaa ya Kinondoni, Mkoani Dar es Salaam, kwa wananchi Takriban 333,584 wenye umri wa kuanzia miaka mitano na kuendelea.

Akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu Ugonjwa wa Matende na Mabusha ili waweze kushiriki katika kuelimisha na kuhamasisha jamii katika zoezi hilo Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambule amesema magonjwa haya yanaweza kuzuilika kwa kupata chanjo/kingatiba ama kupata tiba kwa ambao wanaugua.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Kinondoni Dkt. Samwel Laizer amesema kingatiba hizo zinatarajiwa kutolewa katika kata 10 za wilaya hiyo ambazo ni Kigogo, Mzimuni, Magomeni, Ndugumbi, Tandale, Kijitonyama, Kinondoni, Hananasif, Mwananyamala na Makumbusho kwa watu wote kuanzia miaka mitano na kuendelea.

Nae Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Kinondoni Mhe. Songoro Mnyonge ametoa wito kwa watu wote wenye dalili za ugonjwa wa matende na mabusha wajitokeze kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya ili waweze kutibiwa maana magonjwa hayo yanatibika na kupona kabisa.