Back to top

“Kujiunga upinzani sio jambo rahisi,sumu aionjwi kwa kulambwa”Sumaye

04 December 2019
Share

Waziri Mkuu mstaafu wa awamu ya tatu wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe.Fredrick Sumaye leo ametangaza rasmi kujitoa ndani ya Chama cha Demakrasia na Maendeleo (CHADEMA) baada ya kukaa ndani ya chama hicho kwa miaka minne akitokea chama cha Mapinduzi (CCM).

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Mhe.Sumaye kutangaza kugombea nafasi ya mwenyekiti katika chama hicho na kushindwa kutetea nafasi ya uenyekiti wa chama hicho kanda ya Pwani kwa kupigiwa kura ya hapana.
Mhe. Sumaye amesema nchini Tanzania kujiunga na chama caha upinzani sio  jambo jepesi hasa kwa mtu ambaye ulikuwa kwenye nafasi za juu za utumishi serikalini huku akisema alipata misukosuko mingi sana baada ya uamuzi huo ndani na hata nje ya familia yake.
 
Aidha Mhe.Sumaye ameendelea kueleza kuwa amechukua uamuzi huo kwa kuhofia usalama wake huku akimnukuu mwenyekiti wa chama hicho Mhe.Freeman Mbowe kuwa aliwatahadharisha kuwa sumu haionjwi kwa ulimi hivyo yeye hana sababu ya kuionja hiyo sumu kwa ulimi.

“Nalazimika kujiondoa CHADEMA kuanzia leo, na sijiungi na chama chochote cha siasa, na nipo tayari kutumika kama mshauri wa chama chochote cha siasa” Mhe.Sumaye

Hata hivyo Mhe.Sumaye amesema kuwa amejitoa ndani ya chama na hajiungi na chama kingine chochote hivyo atabaki kuwa mshauri huru kwa chama chochote kitakacho hitaji ushauri kutoka kwake.
Katika hatua nyingine Katibu wa CHADEMA Kanda ya Pwani aliyeongozana na Mhe.Sumaye katika mkutano wake na wanhabari Bw.Casmir Mabina, ametangaza kujiuzulu nafasi yake ya ukatibu ndani ya chama hicho, huku akisema barua ya kujiuzulu tayari kashaiwasilisha kwa uongozi wa juu wa chama hicho.