
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu, ameitaka Tume ya Usuluhishi na Uamuzi CMA kuendelea kukuza matumizi ya teknolojia katika kutatua migogoro ya kazi, ikiwemo kuboresha mfumo wa e-Utatuzi.
Mhe.Sangu ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati wa mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea taasisi zilizo chini ya Ofisi yake, yenye lengo la kufahamu utekelezaji wa majukumu yao, kuimarisha mahusiano ya kikazi, pamoja na kutoa maelekezo ya kuongeza ufanisi, uwajibikaji na tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Amesisitiza kuweka mazingira rafiki kwa watumiaji wa mfumo huo ili uwe nyenzo madhubuti ya kumaliza migogoro kwa wakati na kwa ufanisi, huku akiipongeza Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kwa kufanikisha kusuluhisha migogoro ya kazi 4,339 hadi kufikia Septemba 2025.

Awali akizungumza, Naibu Waziri wa Ofisi hiyo, Mhe. Rahma Kisuo, ameitaka Tume kuendelea kujitangaza na kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma zinazotolewa, pamoja na kuimarisha usawa na haki mahali pa kazi.
Naye Mkurugenzi wa CMA, Bw. Usekelege Mpulla, amesema kuwa Tume itaendelea kuboresha matumizi ya teknolojia ili kuongeza ufanisi katika utatuzi wa migogoro ya kazi.
