
Viongozi wa chama cha ACT Wazalendo wamesisitiza chama hicho kitashiriki chaguzi zote, zitakazofanyika hapa nchini kwa ngazi zote kuanzia uchaguzi wa serikali za Mitaa, inaotarajiwa kufanyika mwaka huu na kusema kazi kubwa walioyonayo kwa sasa ni kutoa elimu ya uraia kwa wananchi ili watambue umuhimu wa kupiga kura na kupata viongozi bora wanaowahitaji.
Katibu Mkuu wa chama hicho Bwana Ado Shaibu, ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa taifa wa chama hicho uliofanyika Jijini Dar Es Salaam na kusema baada ya viongozi wapya kuchaguliwa kazi kubwa ni kutoa elimu ya uraia kwa wananchi ili wajiandae kuchagua viongozi wanaowataka.
Makamu mwenyekiti wa chama cha mapinduzi CCM bwana Abdulhaman Kinana akitoa salamu za mwenyekiti wa CCM, Rais Dokta Samia Suluhu Hassan amesema dhamira ya serikali ni kuhakikisha chaguzi zote zina kuwa huru na haki.
Naye kiongozi wa chama CNL cha nchini Burundi Bw.Agathon Rwasa ameishauri serikali kusikiliza viongozi wa upinzani wanapowasilisha kero na matatizo yanayowakabili wananchi na sio kuwachukuliwa kama magaidi.
Mkutano huo mkuu wa taifa wa ACTA Wazalendo wa siku mbili wenye ajenda kuu ya uchaguzi wa viongozi ndani ya chama hicho ilihudhuriwa na viongozi kutoka ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, na viongozi wa azaki.
