Back to top

AHUKUMIWA KUNYONGWA KWA KUMUUA SHANGAZI YAKE

16 April 2024
Share

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga imemuhukumu mkazi wa Mwigumbi, wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Alex Masanja kunyongwa hadi kufa,  baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumuua shangazi yake Merisiana Malisa, mkazi wa kijiji cha Masagara wilayani humo.

Imedaiwa mahakamani kuwa Alex Masanja, alifanya tukio hilo kwa kukusudia usiku wa tarehe 16/2/2023 majira ya usiku wakati shangazi yake akiwa amelala, ndipo alipommvamia na kumpiga kwa kitu kizito kichwani na kusababisha kifo chake na baada ya hapo aliiba baiskeli ambayo aliiuza siku iliyofuata pamoja na simu na kutoroka kwenda kujificha mkoani Tabora.

Taarifa zinasema Alex alitenda tukio hilo baada ya kukatazwa kutumia baiskeli ya marehemu, kwa kuwa amekuwa akiichukua bila ruhusa na kuirudisha usiku wa manane.

Jaji wa mahakama hiyo Mheshimiwa Sief Kulita amesema ushahidi umeonesha Marehemu alikuwa akiishi na  mjukuu wake  Fatma Deus ambaye ameieleza mahakama kuwa kabla ya mshtakiwa kutekeleza mauaji alikuwa akimpigia simu mara kwa mara akimuuliza Merisiana Malisa anarudi lini nyumbani kwa kuwa alikuwa anamuuguza ndugu yake anayeishi kijiji cha Shilabela, Old Shinyanga.

Wakili wa utetezi Emmanuel Rugamila amesema amekubaliana na hukumu iliyotolewa na mahakama na wakili wa serikali Mboneke Ndimubenya amesema hukumu hiyo ni mafanikio ya kesi zinazohusiana na vitendo vya mauaji ya kikatili.