Back to top

AHUKUMIWA MIAKA 40 KWA MAUAJI YA MWANAFUNZI.

14 December 2023
Share

Naftali Kinuthia mtuhumiwa  mkuu kwenye mauaji ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Moi Ivy Wangeci, amehukumiwa kifungo cha miaka 40 gerezani. 

Jaji Stephen Githinji ametoa hukumu hiyo kwa njia ya mtandao, akiwa katika mahakama ya Malindi anakohudumu sasa.

Ikumbukwe kwamba wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, mahakama ilimkuta Kinuthia  na hatia katika mauaji ya Wangeci ambayo aliyafanya  kwa kutumia shoka mnamo tarehe 9 mwezi Aprili mwaka wa 2019.

Kulingana na jaji Githinji, Kinuthia  alishindwa kuishawishi mahakama kwamba alikuwa katika mahusiano ya kimapenzi na Ivy licha ya Kinuthia kujitetea kwamba alifanya hivyo kwa hasira na hakutaka kumuua Ivy.

Jaji Githinji hata hivyo amesema kwamba iwapo hakuwa na nia ya kumuua Ivy basi angemshambulia marehemu kwa ngumi au makofi badala ya shoka.

Ni zaidi ya miaka minne tangu yatokee mauaji ya Wangeci aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa sita akisomea udaktari katika Chuo kikuu Cha Moi.