
Wakurugenzi wa uzalishaji wa chanjo za mifugo kutoka nchi 25 za Afrika, wamesema uwekezaji uliofanywa na kiwanda cha Hester Biosciences Africa Limited kilichopo katika Eneo la Viwanda la TAMCO, Kibaha Mkoa wa Pwani, ni wa kimkakati na una nafasi kubwa ya kuleta mapinduzi katika sekta ya mifugo si tu nchini Tanzania, bali barani Afrika kwa ujumla.
Mkurugenzi wa AU-PANVAC, Dkt. Bodjo S. Charles, ameipongeza Hester kwa mchango wake mkubwa katika sekta ya afya ya wanyama barani Afrika.
"Tulipofika hapa na kuona majengo haya, tulivutiwa sana na tukatamani kujua kilichomo ndani. Na baada ya kuona teknolojia na miundombinu iliyopo, tumeridhika sana na tunafurahia kuona tuna kituo cha aina hii hapa Afrika. Nina uhakika kiwanda hiki kitatoa mchango mkubwa katika jitihada zetu za kutokomeza ugonjwa wa Sotoka ya Mbuzi na Kondoo (PPR), pamoja na magonjwa mengine ya mifugo, kwa sababu lengo letu siyo kudhibiti PPR pekee, bali pia magonjwa yote ya wanyama,"
"Ninatoa shukrani za dhati kwa uongozi na wafanyakazi wa Hester Biosciences Africa Limited kwa mapokezi mazuri na kwa kutupatia fursa ya kutembelea kiwanda hiki cha kisasa cha uzalishaji wa chanjo za mifugo. Ziara yetu leo imetuthibitishia kwa vitendo kuwa Afrika ina uwezo mkubwa wa ndani wa kuzalisha chanjo bora kwa mifugo, kwa viwango vinavyokubalika kimataifa. Tunavutiwa sana na uwezo wa kiwanda hiki – si tu katika uzalishaji wa kiasi kikubwa cha chanjo, bali pia katika matumizi ya teknolojia ya hali ya juu, viwango vya ubora, na kujitolea kwao kuhakikisha afya ya mifugo barani. Hii ni hatua kubwa kuelekea kujitegemea kama bara katika sekta ya afya ya wanyama."Amesema Dkt. Bodjo
Katika hotuba yake Mkurugenzi wa Hester Biosciences Africa Limited, Bi. Tina Towo Sokoine, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais wa Awamu ya Sita, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa ushirikiano mzuri walioutoa wakati wa ujenzi na uendeshaji wa kiwanda hicho hadi kufikia mafanikio yaliyopo sasa.
"Tuna furaha kubwa kuwa sehemu ya jitihada za bara zima katika kuboresha afya ya mifugo. Ziara ya leo ni ushahidi wa jinsi Afrika inaweza kujenga uwezo wa ndani wa uzalishaji wa chanjo kwa viwango vya kimataifa. Tunajivunia kuwa sehemu ya historia hii na tutaendelea kushirikiana na taasisi kama AU PANVAC katika kutokomeza magonjwa hatarishi kama PPR."
“Kiwanda cha Hester kimeanza rasmi uzalishaji tangu mwaka 2021 na tayari kimeshauza chanjo kwenye nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania, Kenya, Zambia, Botswana, Burundi, Eritrea, Ghana, Mongolia, Nepal na Israeli. Hii inaonyesha mchango wake mkubwa si tu kwa Tanzania, bali kwa afya ya mifugo katika bara zima la Afrika.” Alisema Bi Tina
Wageni waliotembelea kiwanda hicho walipata fursa ya kujionea teknolojia ya uzalishaji ikiwemo njia za Chick Embryo Origin, Tissue Culture, Fermentation, na Continuous Cell Line zinazotumika kuzalisha chanjo salama na bora kwa mifugo. Pato la kila mwaka linatarajiwa kufikia Dola milioni 30 za Kimarekani, huku ajira kati ya 150 hadi 200 zikitajwa kuendelea kutolewa pindi uzalishaji utakapo fikia kiwango cha juu.
Kwa upande mwingine, mkutano wa AU PANVAC unaofanyika katika Ukumbi wa King Jada Hotel, umeweka mkazo katika kuimarisha mfumo wa pamoja wa udhibiti, uzalishaji na usambazaji wa chanjo, hasa kwa ajili ya kutokomeza ugonjwa wa Sotoka ya Mbuzi na Kondoo (PPR). Huu ni ugonjwa hatari unaohatarisha ustawi wa mifugo na uchumi wa wakulima wengi barani Afrika.
Kiwanda hicho, ambacho ni sehemu ya kampuni mama kutoka India Hester Biosciences Limited ni miongoni mwa vituo vya kisasa vya uzalishaji wa chanjo za mifugo barani Afrika ambacho kina uwezo wa kuzalisha dozi bilioni 1.5 kwa mwaka, kikihudumia magonjwa 27 ya mifugo kupitia aina 37 za chanjo, kwa wanyama kama kuku, ng’ombe, mbuzi, kondoo na nguruwe. Uwekezaji wa kiwanda hicho umegharimu Dola za Kimarekani milioni 18, sawa na takriban Shilingi bilioni 44 za Kitanzania.
Ziara hiyo imefanyika kama sehemu ya mkutano wa kikanda wa AU PANVAC unaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 16 hadi 20 Juni 2025.