Back to top

AIRTEL AFRICA YAOKOA MATUMIZI YA LITA MILIONI 9.1 ZA MAFUTA

06 July 2026
Share

Kampuni ya Airtel Africa imefanikiwa kuokoa matumizi ya zaidi ya lita milioni 9.1 za mafuta ya dizeli katika mwaka wa fedha wa 2025/2026, hatua inayotajwa kuimarisha jitihada zake za kulinda mazingira na kukuza biashara endelevu barani Afrika.

Mafanikio hayo yamebainishwa katika Ripoti ya Uendelevu ya kampuni hiyo, ikieleza kuwa yamechangiwa na kupunguza utegemezi wa dizeli pamoja na kuongeza matumizi ya vyanzo vya nishati mbadala vyenye kiwango kidogo cha uzalishaji wa hewa ukaa. Aidha, Airtel Africa imefanikiwa kufunga vituo 390 vya miundombinu vinavyotumia umeme wa gridi na taifa, hatua iliyosaidia kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo jijini Lusaka, Zambia, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Africa, Sunil Taldar, amesema kampuni hiyo inaendelea kuunganisha ukuaji wa biashara na uwajibikaji wa mazingira ili kuhakikisha maendeleo yanayowanufaisha wananchi na jamii kwa ujumla.

Mbali na sekta ya mazingira, ripoti hiyo inaonyesha Airtel Africa imeendelea kuimarisha huduma za kifedha kupitia Airtel Money, ambayo sasa inahudumia wateja milioni 54.1 kupitia mtandao wa mawakala milioni 2.4 katika nchi mbalimbali za Afrika. Takwimu hizo zinaifanya Airtel Money kuwa miongoni mwa mifumo mikubwa ya huduma za kifedha kidijitali barani humo.

Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa asilimia 44.1 ya wateja wa Airtel Money ni wanawake, hali inayotafsiriwa kuwa mchango mkubwa katika kuongeza ushiriki wa wanawake kwenye huduma salama na nafuu za kifedha pamoja na fursa za kiuchumi.

Kupitia taasisi yake ya Airtel Africa Foundation, kampuni hiyo imewekeza zaidi ya Shilingi bilioni 6.2 za Kimarekani katika miradi ya maendeleo ya jamii. Miradi hiyo imejikita katika elimu, ujumuishi wa kifedha, maendeleo ya mazingira na kuimarisha ujuzi wa kidijitali kwa vijana na wanawake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo UNICEF.

Kwa mujibu wa Airtel Africa, hatua hizo zinaakisi dhamira ya kampuni ya kujenga biashara inayochangia maendeleo ya kijamii, ukuaji wa uchumi na uhifadhi wa mazingira, huku ikiendelea kupanua huduma zake za mawasiliano na kifedha katika nchi 14 za Afrika.