AJali ya Basi na Lori yajeruhi 10, wawili kati yao wapo mahututi.

Watu kumi wamejeruhiwa, wawili kati yao vibaya baada basi walilokuwa wakisafiria kugongana na lori katika kijiji cha Darajani, kata ya Inyala mkoani Mbeya.

Ajali hiyo ilihusisha basi la kampuni ya Premier lenye namba za usajili T 629 AET lililokuwa likitokea jijini Mbeya kwenda Mwanza  lililogongana na lori lenye namba za usajili T486 ANU lililokuwa likivuta tela lenye namba za Usajili T775 APT likitokea jijini Dar es salaam kwenda nchini Zambia.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbeya, ambaye pia ni diwani wa kata ya Inyala, Mhe.Mwalingo Kisemba amesema ushahidi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa basi la kampuni ya Premier ambalo lilishindwa kulikwepa lori lililokuwa likiyapita magari mengine yaliyosimama katika eneo hilo.

Dakitari wa Kitengo cha Dharura katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya Dakta Olivia Masoi ambaye amethibitisha kupokea majeruhi kumi amesema watu wawili waliodhaniwa kuwa wamekufa katika eneo la ajali wako hai na wamelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi chini ya uangalizi wa karibu wa madaktari bingwa.