Back to top

ALABAMA KUMUUA MFUNGWA KWA NAITROJENI LEO

25 January 2024
Share

Maafisa wa jimbo la Alabama nchini Marekani wanatazamiwa kumuuwa mfungwa kwa kutumia gesi ya naitrojeni, mbinu ambayo haijawahi kutumiwa hapo kabla.

Kenneth Eugine Smith, mwenye umri wa miaka 58 aliyehukumiwa kwa mauaji, anatarajiwa kuuawa katika gereza moja la Kusini mwa Alabama leo usiku.

Mfungwa huyo alipaswa kuuliwa mwaka wa 2022, kwa kuchomwa sindano ya sumu, lakini tukio hilo likasitishwa dakika ya mwisho, kwa sababu maafisa walishindwa kumuwekea mpira wa kupitisha sumu.

Mawakili wa Smith walipambana mahakamani kusitisha utekelezaji wa adhabu hiyo ya kifo, kwa kutumia naitrojeni, wakihoji kuwa jimbo hilo linataka kumfanya Smith kuwa kesi ya majaribio ya mbinu hiyo mpya ya kuua, ambayo inapaswa kuchunguzwa zaidi kisheria kabla ya kutumiwa kwa mfungwa.

Mahakama ya Juu ya Marekani jana iliikataa hoja ya Smith kuwa itakuwa kinyume cha sheria kufanya jaribio jingine la kumuuwa baada ya lile la kuchomwa shindano kushindwa.