
Mwanamke mwenye umri wa miaka 31 mkazi wa Wanging’ombe aliyekuwa akisumbuliwa na tatizo la uvimbe kwenye kizazi na kupelekea changamoto ya kutoshika ujauzito ambapo alipobahatika kushika ujauzito mimba kutoka mara tatu mfulizo, amefanyiwa upasuaji na Madaktari Bingwa wa Rais Samia.
Hayo yamebainishwa na Daktari Bingwa wa Uzazi na Kizazi Dkt. Chuma Novacatus mara baada ya kufanikisha upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye kizazi uliofanyika katika Hospitali ya Halmashauri ya Wanging’ombe mkoani Njombe
Dkt. Novacatus ameeleza kuwa uvimbe huo umesababisha kusukuma kuta za ndani za kizazi na kutokwa na damu kwa muda mrefu, ambako pia kulimsababishia kupata changamoto ya kutoshika ujauzito, hata alipobahatika kushika ujauzito mimba zilikua zinatoka zinapofikia miezi mitatu au minne.
“ Mama huyo amekuwa akihudhuria katika vituo vya afya mbalimbali na kupatiwa huduma lakini bado hakupata nafuu,” ameeleza Dkt. Novacatus.
Amesema hadi Jumamosi ya wiki iliyopita alipoamua kwenda hospital ya wilaya ya Wanging'ombe- Njombe kwa ajili ya kuendelea na matibabu, ndipo alipopata taarifa ya ujio wa madaktari bingwa wa mama Samia na kuja kituoni hapo.
“Jana kaja hospitali kwa ajili ya kuonana na madaktari bingwa hao, na baada ya kuonwa akafanyiwa uchunguzi wa kina na kugundilika kuwa ana vimbe za kwenye nyumba ya kizazi (uterine fibroids) na kumfanyia upasuaji kutoa uvimbe huo,* ameeleza Dkt. Novatus.
Mama huyo ambaye jina limehifadhiwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ubunifu wa kuwasogezea huduma za kibingwa wananchi wa ngazi ya msingi kwani kwenye ngazi ya msingi ndio wananchi wengi wenye uhitaji wa huduma mbalimbali zikiwemo za kibingwa.
“Nimefurahi sana leo kwani tatizo lililonisumbua kwa muda mrefu limetatuliwa nina imani kuwa sasa niko sawa na kwa uwezo wa Mungu nikijaliwa nitaweza kushika mimba tena na kupata watoto kama ilivyo matamanio yangu na familia yangu,” ameeleza furaha yake.