
Muyengi Ruben mwenye umri wa miaka 25, mkazi wa Kijiji cha Namhula kilichopo wilayani Bunda mkoani Mara, anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo, kwa tuhuma za kumuua Rosemary Malemi, ambaye alikuwa mke wake, huku sababu ikidaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi baada ya ombi la mwanaume huyo kutaka kurudiana na mke wake kukataliwa.
.
Kupitia taarifa iliyotolewa na Jeshi la polisi imebainisha kuwa tukio hilo lilitokea mnamo Januari 20, 2024, majira ya saa 2:00 Asubuhi, katika Kijiji cha Namhula, ambapo Bw.Muyengi Ruben alimfuata Rosemary Malemi shambani alipokuwa anapanda mpunga akiwa na watoto wake, ndipo alipomchoma na kitu chenye ncha kali juu ya titi la kushoto na nyuma ya bega la kulia, hali iliyosababisha kuvuja damu nyingi, kisha kupoteza maisha.
.
Kufuatia tukio hilo Jeshi la Polisi mkoani humo limewataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake wafuate sheria, kanuni na taratibu.
