Back to top

Asilimia 61 ya eneo la Tanzania hatarini kugeuka jangwa.

05 August 2020
Share

Zaidi ya asilimia 61 ya eneo la Tanzania inakabiliwa na hatari ya kugeuka jangwa ikiwa juhudi zaidi hazitachukuliwa kukabiliana na changamoto za uharibifu wa misitu ya asili unaotokana na ongeeko la shughuli za binadamu zisizo endelevu na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Wataalam wa misitu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Timotheo Mande na George Miringay kutoka Ofisi ya RAIS TAMISEMi wameshauri juhudi zaidi ziongezwe katika uhifadhi wa misitu ya asili ili kuinusuru nchi katika hatari ya kugeuka jangwa.

Hayo yamebainishwa katika mkutano wa Wataalam wa Misitu na Mazingira wa kuandaa mkakati wa Tanzania kuhifadhi na kurejesha zaidi ya hekta milioni tano na laki mbili za uoto wa asili chini ya mkakati wa dunia wa Bonn Challenge wa kurejesha hekta milioni 350 ifikapo mwaka 2030.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (WWF) Dk Severin Kalonga amesema WWF Tanzania imekuwa mdau muhimu ikishirikiana na serikali ya Tanzania kutafuta fedha kwa wadau wa kimataifa wa mazingira ili kufanikisha utekelezaji wa mkakati huo muhimu kwa uhifadhi wa misitu.