Back to top

ASKARI 2 WAONESHA UKARIMU KWA WATALII WAPANDISHWA VYEO ARUSHA

17 June 2022
Share

Waziri was Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mhandisi Hamad Masauni amewapandisha vyeo maofisa wawili wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha wanaofanya kazi katika kituo cha Polisi cha Utalii na Diplomasia baada ya kutoa huduma bora kwa watalii.

Akiongea na wanahabari katika kituo hicho cha Polisi, Mhandisi Masauni amewataja aliowapandisha vyeo kuwa ni Mrakibu Msaidizi wa Polisi ASP Waziri Tenga ambaye amepandishwa cheo kuwa Mrakibu wa Polisi (SP) na Mkaguzi wa Polisi INSP Anthony Mwaihoba ambaye amepandishwa cheo kuwa Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP).

Mhe.Masauni ameeleza kuwa alipokea barua toka ubalozi wa Tanzania Nchini Italia ambayo iliandikwa na watalii raia wa Italia waliofika nchini hivi karibuni kwa ajili ya shughuli za utalii.

Waziri Masauni amesema Serikali itandelea kuwathamini na kuwapongeza Askari wote wazalendo na waadilifu wanaotekeleza majukumu yao vizuri popote Nchini.

Sambamba na hilo ametoa wito kwa Askari wengine kufanya kazi kwa uadilifu, uzalendo na kutanguliza maslahi ya Taifa mbele. 

Pia amekemea vitendo viovu kwa baadhi ya Askari wachache ambao sio waadilifu,ambapo amewataka kuacha tabia hizo kwani zinachafua taswira ya Jeshi la Polisi na nchi kwa ujumla.