
Afisa wa Polisi wa kituo cha Nakuru anashikiliwa na naJeshi la Polisi nchini Kenya kwa tuhuma za kusababisha kifo cha muhudumu wa baa (Bar) kwa kufyatulia risasi na kuwajeruhi wengine watatu kufuatia mzozo ulioibuka baada ya kukataa kulipa bili ya vinywaji Ksh.16,000.
Majeruhi hao watatu wanauguza majeraha yao ya risasi katika Hospitali ya Nakuru Level 5.
Katika tukio hilo lililotokea usiku wa saa nane kuamkia Jumatano, Konstebo Nicholas Musau aliripotiwa kujihusisha na mzozo na wafanyabiashara wa baa, katika Klabu ya Vegas na inasemekana alifyatua risasi kabla ya kukimbia.
“..alizua ugomvi na wahudumu wa baa kwenye baa iliyotajwa kuhusu bili za vinywaji alivyokuwa amekunywa. Katika harakati hizo, hali ya taharuki ilitokea na afisa huyo akamjeruhi vibaya mhudumu wa baa ambaye ni Ann Maina,” ripoti ilisema.
Kamanda wa polisi wa Kaunti ya Nakuru alisema afisa huyo alikamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Kaptebwa. Bastola yenye risasi mbili na maganda sita yaliyotumika zilipatikana.
Polisi walisema waathiriwa wanne walikuwa wanaume wawili na wanawake wawili, marehemu alikuwa mwanamke na mwili wake ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha eneo hilo ukisubiri uchunguzi.
