Back to top

Balozi Mbega awataka Wafanyabiashara wa India kuwekeza Tanzania.

14 April 2022
Share

Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Mbega ametoa wito kwa wafanyabiashara wa nchi hiyo kuja kuwekeza Tanzania kwenye sekta mbalimbali za uwekezaji.Ametoa wito huo katika kongamano kubwa la biashara na uwekezaji (Tanzania India Trade Conference) lililofanyika katika jiji la Chennai, India.

Kongamano hilo lililoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ubalozi wa Tanzania nchini India na Taasisi ya Uchumi na Biashara ya India (Indian Economic Trade Organization) lilitoa fursa kwa taasisi mbalimbali zinazohusika na masuala ya uwekezaji na biashara ikiwepo Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwasilisha mada kuhusu fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini.

Balozi Mbega ameeleza kuwa licha ya India kuwekeza nchini mtaji wa kiasi cha Dola za Marekani Bilioni 3.7 na kuifanya nchi hiyo kuwa ya tano kwa uwekezaji, lakini bado nchi hiyo ina fursa kubwa ya kuongeza uwekezaji wake nchini.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na wafanyabiashara na wawekezaji takribani 110 ambapo waliweza kufahamishwa fursa za biashara kwa bidhaa za mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi na fursa za uwekezaji katika sekta za Miundombinu, Madini, Ujenzi wa majumba, viwanda vya madawa, mitambo ya viwandani, nguo, Elimu na Afya.