Back to top

Barabara kuu ya Mbeya-Tabora iliyofungwa kwa wiki mbili yafunguliwa

08 January 2020
Share

Barabara kuu inayounganisha mkoa wa Mbeya na Tabora ambayo ilifungwa kwa wiki mbili kutokana na daraja la mto Lupa kuvunjika na kusababisha mawasiliano kukatika, hatimaye imefunguliwa baada ya ukarabati wa daraja hilo kukamilika.

Mawasiliano ya barabara kati mikoa ya Mbeya, Tabora ambayo yalikatika kwa wiki mbili kutokana na daraja la mto Lupa kuvunjika, hatimaye yamerejea katika hali ya kawaida baada ya wakala wa barabara nchini, TANROADS, kukamilisha ukarabati wa daraja hilo ambalo hivi leo limefunguliwa na mkuu wa wilaya ya Chunya, mhandisi Maryprisca Mahundi kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila.

Kaimu mkurugenzi wa TANROADS mkoa wa Mbeya, mhandisi Magesa Mwita amesema daraja hilo kwa sasa ni imara na linao uwezo wa kupitisha magari yenye uzito usiozidi tani kumi, huku magari ambayo uzito wake ni zaidi ya tani kumi yakitakiwa kuendelea kutumia daraja la chini ambalo limejengwa maalum kwa ajili ya magari ya aina hiyo.

Baadhi ya wananchi wilayani Chunya wameishukuru serikali kwa kukamilisha ukarabati wa daraja hilo kwa madai kuwa kwa kipindi chote ambacho barabara hiyo ilikuwa imefungwa wamepata shida kubwa ya mawasiliano ambayo imeathiri shughuli zao za kijamii na kiuchumi.