
Rais Samia Suluhu Hassan, amependekeza barabara ya mzunguko ya Dodoma ipewe jina la Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dk Akinwumi Adesina, ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake katika maendeleo ya miundombinu nchini.
"Katika kumuwekea Kumbukumbu na kwa kutambua mchango wake na mchango wa Benki ya maendeleo ya Afrika katika kuimarisha sekta ya usafiri na usafirishaji Tanzania, nimeridhia pendekezo la Waziri wa Ujenzi la kuwa barabara hii ya mzunguko ya nje ya Jiji la Dodoma iitwe kwa jina lake. Nitumie fursa hii kutangaza rasmi kuwa barabara hii ya mzunguko nje ya Jiji la Dodoma itaitwa barabara ya Dkt. Akinwumi Adesina." Amekaririwa Rais Samia.
Dkt. Samia amebainisha hayo wakati wa hotuba yake kwa wananchi wa Dodoma mara baada ya kukagua ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa Msalato na barabara hiyo ya mzunguko, akimtakia mema Dkt. Adesina katika mipango yake ya baada ya kustaafu.
"Tanzania imeweza kuvutia mitaji kutoka kwa wabia muhimu kama benki ya Afdb kutokana na kuwepo kwa utulivu na amani, sera nzuri za kiuchumi, usimamizi thabiti wa miradi ya maendeleo na kujituma kwa watanzania wenyewe kujenga nchi yao.
Tumeendelea kuonesha Afrika na Dunia kwamba Tanzania imedhamiria kujenga Taifa lenye uchumi shindani na kustawisha ustawi wa watu wake hivyo niithibitishie Benki ya maendeleo ya Afrika kuwa Tanzania itaendelea kuwa mshirika wa karibu kwaaajili ya kufikia malengo ya bara letu la kuijenga Afrika tunayoitaka na kuleta maendeleo kwa watu wetu" amesema Rais Samia.
Kulingana na Dkt. Adesina ambaye jana alitunukiwa Shahada ya udaktari wa heshima katika sayansi na Chuo kikuu cha Dar Es salaam, Yeye ndiye Rais aliyeitembelea na kufanya kazi kwa ukaribu zaidi na Tanzania, kati ya marais wote waliowahi kuiongoza Benki hiyo tangu mwaka 1971, akifanikisha utoaji wa Mikopo ya Dola za Marekani Bilioni 4.73 kwa kipindi chake cha Miaka kumi ya Uongozi wa Benki hiyo kati ya Dola Bilioni 9 zilizotolewa kwa Tanzania tangu kuanzishwa kwa Benki hiyo ya AfDB.
Dkt. Akinwumi Adesina ni Rais wa 8 aliyechaguliwa wa Kundi la Benki ya Maendeleo ya Afrika. Alichaguliwa kwa mara ya kwanza kwenye wadhifa huo Mei 28, 2015, na Bodi ya Magavana wa Benki hiyo katika Mikutano yake ya Mwaka iliyofanyika Abidjan, Côte d’Ivoire, na kuchaguliwa tena kwa kauli moja mwaka wa 2020.