Back to top

BASHUNGWA: TEMESA BORESHENI HUDUMA KWENYE VIVUKO

22 March 2024
Share

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Lazaro Kilahala kuhakikishia anasimamia masuala ya usalama katika vivuko vyote nchini ili viweze kutoa huduma bora pamoja na kulinda usalama wa mali na abiria.
.
Mhe.Bashungwa ametoa maagizo hayo, leo Machi 22, 2024, wakati akikagua utendaji wa kivuko cha MV Kilindoni kinachotoa huduma za usafiri Wilayani Mafia na Nyamisati Mkoani Pwani, ambapo ametoa wiki moja kwa TEMESA kuhakikisha wanapeleka vichanja vya kuhifadhia shehena za mizigo na bidhaa kwenye kivuko hicho.

“Nitoe maelekezo kwa TEMESA ndani ya wiki moja wawe wamefika hapa na kuleta vifaa vyote vinavyohitajika eneo la mizigo na vipangwe kwa mujibu wa taratibu kwani ni hatari, abiria ana mizigo kusafiri sehemu moja”, amesisitiza Bashungwa.
.
Naye, Mkazi wa Wilaya ya Mafia Bw. Mohamed Mswala ameishukuru Serikali kwa kupeleka kivuko hicho ambacho kimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa Wilaya hiyo na kusema changamoto iliyopo ni kutokuwepo kwa vifaa vya kutosha vya kuhifadhia shehena za mizigo (maturubai na pallet) na kulazimu kupanga mizigo na bidhaa katika maeneo ya kukaa kwa abiria hasa katika vipindi vya mvua.

“Tunashukuru Serikali kwa kivuko hichi lakini tunaiomba Serikali itusaidie kupata vifaa vya kuhifadhia mizigo yetu kwani kuna muda mwingine tunapata kesi ya kulipa mizigo ya watu ambayo tumewasafirishia”, amesema Bw. Mohamed.