
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde, amebainisha kuwa programu ya kujenga kesho iliyo njema kwa wajasiriamali wanawake na vijana, kupitia sekta za Mifugo na Uvuvi (BBT-LIFE) itakuwa chachu ya mabadiliko kwa wafugaji kuachana na mtindo wa kuchunga na kuingia kwenye mfumo wa ufugaji wa kisasa.
Mhe.Silinde amebainisha hayo mkoani Morogoro alipotembelea Maonesho ya wakulima, wafugaji na wavuvi (NaneNane) kanda ya Mashariki ambapo amesema kuwa vijana watakaohitimu kwenye kila awamu kupitia programu hiyo watakuwa mabalozi wazuri watakaporejea kwenye maeneo yao.
"Watu wengi huamini baada ya kuona na ndio maana na sisi tunaamini kupitia mafunzo ya ufugaji wa kisasa wanayopatiwa vijana hawa, wafugaji wengi wanaoendelea na ufugaji wa kuchunga wataenda kubadilika hasa baada ya kuona tija inayopatikana kupitia ufugaji wa kisasa" Amesisitiza Mhe. Silinde.
Wakati huo huo Mhe.Silinde amebainisha kuwa Serikali kupitia Wizara za Kilimo na Mifugo na Uvuvi inakusudia kushirikisha nchi jirani kwenye Maonesho ya kitaifa ya Wakulima, wafugaji na wavuvi (NaneNane) kuanzia Mwakani.
"Tumeamua kufanya hivyo ili kuwapa fursa wadau wa sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi waliopo kwenye nchi hizo kuja kuonesha namna wanavyotekeleza shughuli hizo kwenye nchi zao na kutoa fursa kwa watu wetu kupata bidhaa mbalimbali kutoka huko" Amesema Mhe. Silinde.
Ameongeza kuwa hatua hiyo pia itawapa fursa wakulima, wafugaji na wavuvi waliopo nchini kupata jukwaa la kuuza bidhaa zao kwa wadau wa sekta hizo kutoka nchi jirani.
Maonesho ya kitaifa ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi kwa mwaka huu yanabebwa na kauli mbiu isemayo "Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo endelevu ya Chakula.




