Back to top

Benki ya Dunia yaahidi kuisaidia Tanzania kukabiliana na athari cOrona

29 September 2021
Share

Benki ya Dunia imeahidi kuisaidia Tanzania kukabiliana na athari za kiuchumi  zilizosababishwa na ugonjwa wa UVIKO - 19, kutekeleza miradi itakayosaidia kukuza ajira kwa vijana, kuboresha miundombinu ya afya na elimu na kuendeleza rasilimali watu.

Makamu wa Rais wa Benki hiyo, Dakta Hafez Ghanem ametoa ahadi hiyo jijini Dodoma katika mazungumzo yake na  Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwigulu Nchemba.

Ameyataja maeneo ambayo benki hiyo itasaidia kuwa ni ukosefu wa  ajira hususani kwa vijana kwa kuwekeza katika mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kuimarisha sekta ya nishati ya umeme, kuboresha miundombinu ya usafirishaji na kuimarisha sekta binafsi, ili iweze kuchangia katika kutoa ajira na kukuza uchumi wa nchi.

Kwa upande wake, Mhe. Nchemba ameishukuru benki hiyo kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ile mitano iliyosainiwa hivi karibuni  inayogharimu zaidi ya shilingi trilioni moja nukta tatu.