Back to top

BILIONI 44.14 KUWASHA UMEME HANDENI NA KILINDI

13 February 2026
Share

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba leo Februari 12, 2026 amekagua na kuweka jiwe la msingi la Mradi wa ujenzi kituo cha kupokea na kupoza umeme cha MVA 60 Mkatata Tanga na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa  kilovolti 33.

Akiweka jiwe la msingi mradi huo, Dkt. Mwigulu amesema kutekelezwa kwa mradi huo ni jitihada za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika. 

"Nitoe rai kwa Wizara ya Nishati kuhakikisha kasi ya ukamilishwaji wa mradi huo na unakamilika kwa wakati ". Amesisitiza Mhe. Waziri Mkuu. 

Katika hatua nyingine ameiagiza Wizara ya Nishati kuwasiliana na Wizara ya Fedha ili kukamilisha malipo ya fidia kwa Wananchi takribani shilingi bilioni moja.

Ujennzi wa mradi huo ni shilingi bilioni 44 na unahusisha ujenzi wa vituo viwili vya kupokea, kupoza na kusambaza umeme vyenye uwezo wa MVA 60 huku kila kimoja kikiwa na MVA 30,  pamoja na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 33 kutoka kituo cha Mkata hadi kwa Msisi.

Kwa upande wake Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amemshukuru Mhe. Rais kwa kuwezisha upatikanaji wa fedha zitakazo tumika katika utekelezaji wa mradi huo.

“Utekelezaji wa mradi huu unakwenda kuondoa changamoto za umeme katika Wilaya za Handeni na Kilindi ambazo zinapata umeme kutokea Tanga mjiani ambapo ni umbali mrefu". Amesema Mhe. Ndejembi. 

Amefafanua kuwa kupitia miundombinu hiyo mipya, umeme utasafirishwa kutoka Mkata kwenda Msisi kwa umbali wa kilomita 45, hatua itakayoongeza uwezo wa usambazaji na kuimarisha huduma katika maeneo hayo.

Kuimalika kwa huduma ya umeme Wilaya za Handeni na Kilindi kutachochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii.