Back to top

USHAHIDI MPYA KESI YA UHAINI LISSU AIBWAGA JAMHURI

30 July 2026
Share

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amemshinda Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) baada ya Mahakama ya Rufani Tanzania kutupilia mbali ombi lake la kutaka kuongeza ushahidi mpya katika kesi ya tuhuma za uhaini inayomkabili.
 
Uamuzi huo umetolewa na jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo ya rufani ambao ni Jaji Augustine Mwarija, Jaji Zahara Muruke na Jaji Amour Khamisi, baada ya kukubaliana na uamuzi uliyotolewa na jopo la majaji watatu wa mahakama kuu masjala ndogo Dar es Salaam, Jaji Dunstan Ndunguru akisaidizana na Jaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.

Akitoa uamuzi huo, Jaji Mwarija amesema kutokana na hoja zinazokinzana zilizowasilishwa na pande zote, suala linalopaswa kuamuliwa na mahakama hiyo ni kama, badala ya kujadili uhalali wa notisi, mahakama ya mwanzo ilijadili na kukataa ushahidi wa nyongeza uliokusudiwa bila kumpa mwombaji haki ya kusikilizwa kuhusu kukubalika  kwa ushahidi huo.

Amesema ili kujibu suala hilo, wanaanzia kwenye hati ya kiapo iliyowasilishwa kuunga mkono maombi pamoja na sehemu husika ya mwenendo wa shauri katika mahakama ya mwanzo (mahakama kuu) ambao ni sehemu ya kumbukumbu ya maombi hayo.

Amesema upande wa Mashtaka ulipata taarifa hiyo wakati ukiandaa ushahidi wa shahidi huyo ili kutoa Ushahidi Februari 22, 2026 na Bwana Lissu alipinga ombi la upande wa mashtaka akidai kuwa mwombaji alikuwa anataka kuwasilisha ushahidi mpya, ilihali kifungu ambacho notisi hiyo imeongezwa kinahusu kumwita shahidi ambaye taarifa yake au muhtasari wa ushahidi wake haukusomwa wakati wa mwenendo wa kupeleka shauri mahakama kuu.

Jaji Mwarija amefafanua vifungu hivyo, amesema kifungu 308(1) shahidi ambaye taarifa yake au muhtasari wa ushahidi wake haukusomwa wakati wa mwenendo wa kukabidhi mahama hataruhusiwa kuitwa na upande wa mashtaka kutoa ushahidi wakati wa kesi, isipokuwa upande wa mashtaka uwe umetoa taarifa ya maandishi ya kutosha kwa mshtakiwa au wakili wake kuhusu nia ya kumwita shahidi huyo.

Jaji Mwarija amesema mbali na kuomba maombi hayo yatupiliwe mbali, Lissu aliomba pia alipwe fidia kwa madai kwamba maombi haya yaliwasilishwa bila msingi, kwa nia ya kuchelewesha uamuzi wa shauri la jinai.

Hatua hiyo imefikia baada ya  Mahakama kuu ya Tanzania, Masijala Ndogo ya Dar es Salaam, kusimamisha kuendelea kwa kesi ya uhaini inayomkabili Bwana Tundu Lissu kufuatia mawakili wa upande wa Jamhuri kuwasilisha maombi ya mapitio ya kesi hiyo ya uhaini katika mahakama ya juu ya Rufaa ya Tanzania.