Back to top

Bilioni 5 kutumika kulinda hifadhi za bahari nchini.

18 May 2022
Share

Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) wamekubaliana kutekeleza mradi wa kulinda na kutunza baianuai ya ukanda wa Bahari ya Hindi katika Wilaya ya Mkinga iliyopo mkoani Tanga.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amebainisha hayo baada ya kufanya kikao kifupi na Mwakilishi wa shirika hilo nchini Dkt. Katrina Bornemann kilichofanyika ofisini kwake jijini Dodoma.

Amesema lengo la mradi huo ambao utagharimu shilingi za kitanzania bilioni 5 ni kuhakikisha maeneo ya bahari pamoja na ukanda wa pwani Wilayani Mkinga yanalindwa na kuhifadhiwa ili yaweze kuwa endelevu na kuleta maendeleo kwa wananchi.

Ameongeza kuwa wameshakubaliana mradi huo utaanza mara moja na tayari shirika hilo limeshaidhinisha kiasi hicho cha pesa kitumike katika mradi huo utakaodumu kwa miaka 5.

"Tunalishukuru shirika hili la GIZ kwa kuamua kushirikiana nasi katika kutunza baianuai ya bahari nchini, ahadi yetu ni kuwa tutatekeleza mradi huu kwa ustadi na weledi mkubwa kuhakikisha kwamba matokeo yanayotarajiwa yanapatikana na yanaonekana hasa kwa wananchi wetu ambao wataguswa na mradi huu" amebainisha Mhe. Mashimba Ndaki.

Mwakilishi wa shirika hilo la GIZ hapa nchini, Dkt. Katrina Bornemann alifika jijini Dodoma kuonana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa lengo la kuutambulisha mradi huo ili uweze kuanza kutekelezwa mapema kama ilivyokusudiwa.