Back to top

BIMA YA AFYA KWA WOTE AHUENI KWA WANANCHI

08 January 2023
Share

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi, Wizara ya Afya , Idara ya Kinga ,Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma , Dokta Tumaini Haonga amesema, Bima ya Afya kwa Wote itawezesha wananchi kuwa na uhuru wa kupata huduma za matibabu katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya hapa nchini.

Dokta Haonga amebainisha hayo Jijini Mwanza ikiwa ni katika hatua za uhamasishaji kwa wananchi umuhimu wa Bima ya Afya kwa wote katika utekelezaji wa agizo la katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof.Abel Makubi, la kuhakikisha kila taasisi za kisekta zinakuwa na nguvu ya pamoja katika utoaji wa elimu.

Aidha Dokta Haonga ametoa wito kwa wananchi wote kuchangamkia fursa ya Bima ya Afya kwa Wote kwani itarahisisha kupata uhakika wa matibabu kabla ya kuugua.

Naye Mjumbe wa Sekretarieti ya Bima ya Afya kwa Wote kutoka Wizara ya Afya Jackline Tarimo, amesema Bima ya Afya kwa wote itarahisisha kwa mwananchi kupata matibabu bila kikwazo kwani kwa sasa kuna asilimia 85 ya wananchi wasiokuwa na uhakika wa kupata matibabu.

Muswada wa sheria wa Bima ya Afya kwa Wote unatarajiwa kusomwa Bungeni mwishoni mwa mwezi huu Januari 2023 na iwapo utapitishwa utaanza kufanya kazi rasmi Mwezi Julai, 2023 kama sheria ya Bima ya Afya kwa wote.