Back to top

Bobi Wine aitisha maandamano kupinga matokeo ya uchaguzi Uganda.

22 January 2021
Share

Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine, ameitisha maandamano ya amani nchini humo kupinga kile amedai kuwa wizi wa kura katika uchaguzi wa wiki iliyopita, uliompa ushindi rais Yoweri Museveni.

Akizungumza kupitia ukurasa wake wa Youtube kutoka nyumbani kwake anakozuiliwa na wanajeshi wa Uganda UPDF, Bobi Wine ametaka wafuasi wake kujitokeza kwa wingi kote nchini na kuandamana kwa amani, bila kuvunja sheria yoyote, akisema kwamba kwa kufanya hivyo, watakuwa wanadai haki yao ya kikatiba.

Amesema kwamba hatakubali kunyamazishwa na polisi ambao wamemtaka kusema wazi kwamba hataitisha maandamano.

“Nimesikia polisi wakiniambia kwamba niwaambie watu wangu wasifanye maandamano ndipo waniachilie huru. Hilo sio jukumu langu. Raia wa Uganda wanajua kwamba hawajavunja sheria yoyote.”

Bobi wine amesisitiza kwamba alishinda uchaguzi mkuu uliofanyika Januari 14 mwaka huu 2021.

Tume ya uchaguzi ilimtangaza rais Museveni kuwa mshindi wa uchaguzi huo kwa asilimia 58.64 ya kura zilizopigwa. Bobi Wine alipata asilimia 34.83.

Bobi Wine, amedai kwamba chama chake cha National Unity Platform, kina ushahidi wa kutosha kwamba udanganyifu mkubwa wa kura ulifanyika na kumpa ushindi rais Museveni.

#VOA