Back to top

Bodi ya Korosho yakanusha Salfa kukausha maua ya Korosho.

20 October 2020
Share

Bodi ya korosho nchini imesema kukauka kwa maua ya mikorosho katika mikoa ya Mtwara, Lindi na baadhi ya maeneo ya mkoa wa Ruvuma kunatokana na mabadiliko ya hali ya hewa na si matumizi ya Salfa.

Kaimu Mkurugenzi wa bodi ya Korosho nchini Alfred Francis ametoa ufafanuzi huo baada ya kuzagaa kwa taarifa kwenye mitandao ya kijamii ikieleza mikorosho inakauka kutokana na matumizi ya salfa.

Kaimu Mkurugenzi wa bodi ya Korosho nchini Alfred Francis.

Amesema kutokana na mabadiliko ya tabia nchi kumesababisha  kushuka kwa joto chini ya nyuzi joto ishirini na kufikia nyuzi joto kumi na saba mwezi wa saba na wa nane ndio sababu kubwa iliyopelekea maua ya korosho kukauka.

Kufutia hilo amewataka baadhi ya watu kuacha tabia ya kuweka ujumbe mitandaoni pasipo kutafuta ukweli huku akisisitiza matumizi ya salfa katika zao la korosho yameleta faida kubwa.

Amesema uzalishaji wa zao la korosho umekuwa ukipanda kila msimu kutokana wakulima kutambua umuhimu wa kutumia pembejeo ili kuzalisha korosho kwa kiwango kikubwa.

Hata hivyo amesema matumizi ya salfa katika mikoa hiyo yameweza kupandisha uzalisaji wa zao la korosho na kusisitiza matarajio ya mwaka huu ni kuona uzalishaji unaongezeka kutoka tani laki mbili na elfu thelathini na mbili msimu uliyopita na matarajio ya msimu  huu ni  kufikia tani laki mbili na elfu sabini na nane elfu.