Back to top

Brigedia Jenerali Mbungo ateuliwa kuwa Mkurugenzi TAKUKURU.

26 March 2020
Share

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 26 Machi, 2020 amepokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2018/19 na ripoti ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ya mwaka 2018/19, Ikulu Chamwino, Mkoani Dodoma.

Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bw. Charles Kichere kwa kazi nzuri ya ukaguzi aliyoifanya ambayo imeonesha maeneo mbalimbali ambayo Serikali imefanya vizuri na maeneo ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi, na amewaagiza Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi kwenda kufanyia kazi dosari zote zilizojitokeza katika utendaji kazi wa Serikali.

Pamoja na kupokea ripoti 19 za ukaguzi kutoka kwa CAG, amempongeza kwa ofisi yake kuanza kukagua mashirika ya umma badala ya kutumia taasisi za ukaguzi za nje ya nchi hali iliyowezesha kuokoa shilingi Bilioni 1.4, kuonesha dosari za matumizi ya fedha katika taasisi mbalimbali ikiwemo vyama vya siasa na Jeshi la Polisi.

Rais Magufuli amempongeza na kumteua Brigedia Jenerali John Mbungo aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa TAKUKURU kuwa Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo kwa kazi nzuri katika kudhibiti vitendo vya rushwa, kuokoa fedha na mali za umma zilizokuwa zimepotea, na pia kurejesha shilingi Bilioni 8.8 za wakulima zilizokuwa zimeibwa kupitia vyama vya ushirika vya wakulima hapa nchini.