
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Abdallah Ulega amesema Wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo wamejipanga kuhakikisha malighafi za kutengenezea chakula cha kuku ikiwemo mahindi na soya zinapatikana kwa urahisi na kwa bei nafuu ili kupunguza gharama za uzalishaji.
"Kwa upande wa chakula cha kuku tumejipanga kwa kushirikiana na Wizara ya kilimo, wachakataji na wauzaji wa chakula cha kuku kutafuta suluhu ya jambo hili, hatutaki kuona mahindi na soya vinakuwa ni tatizo kwa wachakataji na wauzaji wa chakula cha kuku"Amesema Ulega.
Ulega ametoa kauli hiyo alipotembelea Kiwanda cha Interchick kuona shughuli za uzalishaji wa chakula cha kuku na utotoleshaji wa vifaranga katika Kiwanda hicho kilichopo Wilayani Kinondoni Jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa wanataka kuwapa kipaumbele Wadau hao kwa sababu tasnia hiyo ina uwezo wa kuajiri watu wengi na kuzalisha chakula cha kutosha chenye uhakika wa protini ambacho kitasaidia kujenga jamii yenye afya bora na nguvu.
Ameongeza kuwa katika jitihada za kutatua changamoto zinazoikabili tasnia hiyo, Wizara yake imepanga kukutana na wadau wote wanaojihusisha na mnyororo wa thamani wa zao la kuku ili kujadiliana na kuweka mipango madhubuti ya kutatua changamoto zao na waweze kufanya shughuli zao kwa gharama nafuu na wapate faida.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe.Godwin Gondwe amemueleza Waziri Ulega kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni imetenga kiasi cha shilingi bilioni 3.9 kutoka katika asilimia kumi ya mfuko wa kuwezesha vijana, kina mama na watu wenye ulemavu ili kuwezesha vikundi vya ujasirimali Wilayani humo.
"Mhe.Naibu Waziri, sisi Wilaya ya Kinondoni tumetenga kiasi cha pesa kisichopungua Milioni 150 kutoka katika asilimia kumi iliyotengwa kuwawezesha wajasirimali na tutawapatia vikundi nane (8) vya wafugaji wa kuku,"Amesema Gondwe.
Awali, Mkurugenzi wa Kampuni ya Interchick, Nelson Kikolea alimueleza Naibu Waziri Ulega kuwa upatikanaji wa nafaka ya mahindi na soya umekuwa ni changamoto kubwa na kusababisha gharama za uzalishaji kuongezeka na wanaoathirika zaidi ni wafugaji wadogo wadogo.
Amesema kuwa bei ya mahindi mwaka jana ilikuwa shilingi 460 lakini mwaka huu imepanda mpaka shilingi 940 kwa kilo moja ikiwa ni ongezeko la shilingi 300.
