
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira, Mh.Khamis Hamza Chilo, amewataka viongozi wa mikoa na wilaya nchini, kwenda kuwafundisha wananchi namna bora ya kusimamia sheria na taratibu za utunzaji na uhifadhi wa vyanzo vya maji.
Pia ametaka viongozi hao kuelimisha namna ya kufuata na kutekeleza sheria zitakazolinda mazingira, ardhi na maliasili wakiwemo wanyama pori na mapori ya akiba.
Chillo ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na uongozi wa mkoa wa Simiyu pamoja na wananchi wa kata ya Ihusi-Bariadi, Mkoani Simiyu katika mkutano wa hadhara wakati kamati ya mawaziri 8 wa kisekta wanaoshughulikia migogoro ya Ardhi ya Vijiji 975.
Amesema miongoni mwa vitu vikubwa ambavyo Kamati ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta imebaini wakati wa ziara zake ni upungufu na uchache wa usimamizi wa seheria hasa zile sheria za mazingira.
Kwa mujibu wa Chillo moja ya njia sahihi ya kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi bila kuleta taharuki kama ilivyoelekezwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ni kwenda kuwafundisha wananchi kipi kipo kwenye sheria.

