Back to top

UHAMASISHAJI MATUMIZI SAHIHI YA CHANJO ZA MIFUGO NJOMBE NA IRINGA

28 May 2026
Share

Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), kupitia Sehemu ya Mipango, Masoko na Habari, imeendelea kuimarisha utoaji wa elimu kuhusu matumizi sahihi ya chanjo za mifugo kwa kufanya ziara ya uhamasishaji katika mikoa ya Njombe na Iringa.

Ziara hiyo iliyofanyika kuanzia tarehe 21 hadi 24 Mei, 2026, ikiongozwa na Afisa Habari Mwandamizi wa TVLA, Bw. Daudi Nyingo pamoja na Afisa Masoko, Bw. Fihiri Mbawala, ikiwa na lengo la kuwajengea uwezo wauzaji wa chanjo pamoja na wadau wa sekta ya mifugo kuhusu matumizi sahihi ya chanjo zinazozalishwa na TVLA.

Katika Mkoa wa Njombe, timu hiyo ilitembelea maduka ya pembejeo za mifugo yanayouza chanjo za TVLA yaliyopo katika Halmashauri ya Mji wa Njombe, Makambako pamoja na Wilaya ya Wanging’ombe, na kwa upande wa Mkoa wa Iringa, ziara hiyo ilifanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Mafinga, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa na Manispaa ya Iringa.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Bw. Nyingo alisema TVLA inaendelea kutoa elimu kwa wadau mbalimbali ili kuhakikisha chanjo zinazozalishwa zinatumika kwa usahihi na kutoa matokeo yaliyokusudiwa kwa wafugaji.

"Lengo letu ni kuhakikisha wauzaji wa chanjo wanapata elimu sahihi kuhusu namna bora ya kuhifadhi chanjo, usafirishaji wake pamoja na matumizi yake ili kuendelea kulinda afya ya mifugo na kuongeza tija kwa wafugaji" Asema Bw. Nyingo.

Kwa upande wake, Bw. Mbawala alisema kuwa TVLA inaamini kuwa wauzaji wa chanjo ni kiungo muhimu kati ya taasisi na wafugaji, hivyo wanapaswa kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu bidhaa wanazouza.

"Tunawahimiza kuendelea kufuata maelekezo ya kitaalamu kuhusu utunzaji wa chanjo ili kuhakikisha ubora wake unabaki salama hadi unapomfikia mfugaji" Amesema.

Baadhi ya wauzaji wa chanjo waliotembelewa walieleza kufurahishwa na elimu waliyoipata kupitia ziara hiyo, wakisema itawasaidia kuboresha huduma kwa wateja wao pamoja na kuongeza ufanisi katika matumizi ya chanjo.

Ziara hiyo ni sehemu ya mkakati endelevu wa TVLA wa kuimarisha matumizi sahihi ya chanjo za mifugo nchini, sambamba na kuendelea kuwafikia wadau mbalimbali wa sekta ya mifugo kwa lengo la kuongeza uzalishaji na kuchochea maendeleo ya sekta hiyo.