Back to top

Corona yaweka maisha ya watu rehani, Zaidi ya watu 2,400 wafariki.

24 February 2020
Share

Mamlaka nchini Italia zimelifuta tamasha maarufu la kanivali katika mji wa kitalii wa Venice, kwa hofu ya kusambaa kwa kirusi cha Corona, ambacho hadi sasa kimewashaambukiza watu 150 katika taifa hilo la kusini mwa Ulaya. 

Watu watatu wanatajwa kupoteza maisha kwa ugonjwa wa COVID-19 unaotakana na kirusi hicho katika jimbo hilo na jengine la Lombardy, yote yakiwa kaskazini mwa Italia. 

Austria ilizuia kwa muda wa masaa manne safari za treni kutoka Italia, kwa kile ilichosema ni kujipanga kukabiliana na uwezekano wa maambukizi kuingia kwenye mipaka yake. 

Aidha Iran imethibitisha vifo vya watu wanane kutokana na ugonjwa huo, huku mataifa jirani yakifunga mipaka yao na taifa hilo la Ghuba ya Uajemi. 

Nchini China, ambako ndiko ugonjwa ulikoanzia, Rais Xi Jinping amesema kirusi hicho ni dharura kubwa kabisa ya kiafya kuwahi kulikumba taifa hilo tangu kuundwa kwake mwaka 1949. 

Hadi sasa, watu zaidi ya 2,400 wameshapoteza maisha na wengine 80,000 wameshaambukizwa duniani, wengi wao wakiwa ndani ya China.