Back to top

DAR YAONGOZA WAGONJWA WA RED EYES, WAFIKIA 6,412

08 February 2024
Share

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba, Wizara ya Afya, Prof. Paschal Ruggajo amesema Mkoa wa Dar es Salaam ndio unaongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi wa Red Eyes, ambapo hadi sasa wamefikia wagonjwa 6,412, ukifuatiwa na Pwani wagonjwa 4,041, Dodoma 363, Morogoro 307, Mtwara 193, Shinyanga 193, Tanga 190 na Lindi 101.
.
Prof.Ruggajo ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za Wizara hiyo, zilizopo Jijini Dar es Salaam, ambapo amewataka wananchi kuacha tabia ya kutumia dawa za macho zisizo rasmi kwa lengo la kutibu ugonjwa huo, kwani inaweza kusababisha upofu usiotibika.
.
Prof.Ruggajo amesema Baadhi ya vitu ambavyo watu wamekuwa wakivitumia ni pamoja na dawa zenye vichocheo vya ‘steroids’ ambazo wananunua wenyewe kwenye maduka ya dawa, tangawizi, chai ya rangi illiyokolea majani, mafuta tete yaliyokuwa yakitumika wakati wa janga la Covid - 19, maji ya chumvi na maziwa ya mama, ambavyo vitu vyote hivyo sio salama na havijaelekezwa na wataalamu.
.
Aidha, Wizara hiyo imeendelea kuisisitiza jamii kuzuia kuenea kwa maambukizi ya Red Eyes kwa kuzingatia usafi binafsi na kanuni za Afya ikiwa ni pamoja na Usafi wa mikono na uso, na kuzuia kugusa macho yako kadri uwezavyo.