Back to top

DARAJA LA JPM LAFIKIA 85%, KUKAMILIKA DISEMBA 2024.

15 March 2024
Share

Ujenzi wa Daraja la Kigongo - Busisi, maarufu kama daraja la JPM, linalojengwa kuunganisha Barabara Kuu ya Usagara - Sengerema - Geita, katika Ziwa Victoria umefika asilimia 85 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Disemba, 2024.

Taarifa hiyo imetolewa  katika ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Selemani Kakoso  ilipoambatana na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa kukagua maendeleo ya mradi huo mkoani Mwanza.

Kakoso ameiagiza  Wizara ya Ujenzi kuimarisha mifumo ya ulinzi na usalama katika daraja hilo ambalo linatokana na kodi za wanachi ili liweze kudumu kwa muda wa miaka 100.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema mpaka sasa jumla ya Shilingi Bilioni 441.3 zimetolewa kwa ajili ya kumlipa Mkandarasi anayetekeleza mradi huo.

Awali akitoa taarifa ya mradi, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Eng. Doroth Mtenga ameeleza kuwa mradi huo unatumika kama darasa la mafunzo kwa wanafunzi na wataalamu wetu wa ndani kupata uzoefu wa kusimamia na kujenga madaraja mengine kama hayo hapa nchini.