Back to top

DAWA ZA KULEVYA NDANI YA PIPI ZAKAMATWA ZNZ

02 March 2026
Share

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar kwa kushirikiana na Kikosi Kazi cha Kupambana na Uhalifu Mkubwa wa Kupangwa (ZTOCTF) imefanya Operesheni Maalum kwa lengo la kudhibiti usambazaji wa dawa za kulevya ambazo zinasambazwa kwa kutumia mbinu mpya ya kuzichanganya katika bidhaa za kawaida za matumizi ya kila siku. 

Operesheni hiyo iliyofanyika Januari 25 na 29, 2026, katika maeneo ya Paje, Jambiani, Mbweni, na Shangani, ilifanikiwa kukamata kilo 7.448 za bidhaa kama pipi, chokoleti, korosho, na shisha (electronic cigarettes) zilizochanganywa na viambata vya Bangi, Cocaine, na LSD.

Uchunguzi umebaini kuwa dawa hizo zinaingizwa nchini na raia wa Romania, Alexandru Rozescu, kupitia kampuni ya “Zebra Retail Investment” na kusambazwa hadi nchi jirani za Kenya, Uganda, Rwanda, Zambia, na Malawi. 

Mtuhumiwa huyo tayari amefikishwa Mahakamani pamoja na Watanzania wawili, Nahid Bandar Imtiz na Farhad Mustafa Gulam, huku vyombo vya usafiri vikiwemo magari matatu na pikipiki sita vilivyotumika katika uhalifu huo vikikamatwa.

Wahalifu hao wanatumia vifungashio vyenye muonekano wa kuvutia na ladha mbalimbali kama Grape Ice na Bubble Gum ili kuwalenga watoto chini ya miaka 18 na vijana bila wao kutambua hatari iliyomo. 

Mamlaka imeonya kuwa bidhaa hizo zinaweza kusababisha madhara makubwa ya kiafya ikiwemo changamoto za akili, mshtuko wa moyo, kansa ya mapafu, na vifo vya ghafla, huku ikisisitiza kuwa haitavumilia vitendo hivyo vinavyoharibu nguvu kazi ya taifa.

Serikali imetoa wito kwa wazazi na walezi kuwa makini na bidhaa wanazonunulia watoto wao, hasa zile zenye vifungashio visivyozoeleka, na kuwataka wananchi kutoa taarifa za siri kupitia namba ya bure 119. 

Mamlaka imewahakikishia wananchi kuwa itaendelea kusimamia sheria na kuchukua hatua kali dhidi ya wote wanaohusika na mtandao huu wa dawa za kulevya bila kujali utaifa au madaraka yao.