Makamu wa Rais, Mhe. Dk. Philip Isdor Mpango, ameipongeza Wizara ya Nishati kwa usimamizi madhubuti wa miradi mbalimbali ya Sekta ya Nishati hususan miradi ya umeme ambayo inapelekea nchi kuzidi kujiimarisha kiuchumi.
Dk. Mpango ametoa pongezi hizo wakati alipokagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha umeme wa msongo wa Kilovoti 132 kutoka Tabora hadi Kigoma yenye urefu wa Kilomita 395 pamoja na ujenzi wa kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme cha Nguruka na na Kidahwe vilivyoko mkoani Kigoma.
Akiwa kwenye kituo cha kupoza umeme cha Nguruka ambacho ujenzi wake umefikia asilimia 95, Dkt. Mpango ameiagiza Wizara ya Nishati kupitia TANESCO kuhakikisha ifikapo mwezi Septemba mwaka huu Kigoma iwe imeungwa kwenye Gridi ya Taifa ya umeme na hivyo kutatua changamoto ya upatikanaji wa umeme ambao umekuwa ukirudisha nyuma shughuli za uwekezaji kwenye mkoa huo.
‘’Nimpongeze Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko kwa kuisimamia vyema sekta hii, na pia niwapongeze sana TANESCO kwa kazi nzuri mnayofanya ila ni muhimu sasa mkahakikisha Mkoa wa Kigoma unaingia kwenye Gridi ya Taifa ili kuufungua mkoa huu kiuchumi."Makamu wa Rais, Mhe. Dk. Philip Isdor Mpango.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amemshukuru Makamu wa Rais, kupitia Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha za kutosha kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali hususan mradi wa ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Nguruka na kuahidi kuendelea kusimamia miradi ya nishati ili kuhakikisha umeme unapatikana kwa uhakika kwa wananchi.
‘’ Nikuhakikishie Mhe Makamu wa Rais sisi Wizara ya Nishati tunakuhakikishia kuwa hatutakuwa kikwazo kwa wananchi kupata umeme bali tunaahidi kuwapatia umeme wa uhakika watanzania wote’.’ Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga.
Ameongeza kuwa Wizara itaendelea kutekeleza miradi ya umeme ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa mradi wa umeme wa Igamba Kidahwe hadi Malagarasi ambapo mpaka sasa mkandarasi ameshakabidhiwa eneo la mradi.
Mradi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 132 kutoka Tabora hadi Kigoma na kituo cha kupoza umeme cha Nguruka unatekelezwa na mkandarasi kampuni ya TBEA kutoka China na unagharimu kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 12 na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Kidahwe kitakachopokea umeme kutoka Nyakanazi unagharimu shilingi bilioni 5 na unatekelezwa na wataalam wa ndani kutoka TANESCO.
.
Ujenzi huo ukikamilika utaunganisha Wilaya nne za Mkoa wa Kigoma ambazo ni Kigoma Mjini, Buhigwe, Uvinza na Kasulu na pia kuongeza hali ya upatikanaji wa umeme kwa mkoa wa Kigoma kupitia Gridi ya Taifa.