
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Emmanuel Nchimbi amemuelekeza Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba kuiwezesha Wizara ya Ujenzi kiasi cha Shilingi Bilioni 1.8 kwa ajili ya malipo ya fidia kwa wananchi waliopisha mradi wa upanuzi wa njia nne wa barabara ya Bukoba Mjini kuanzia Rwamishenye Roundabout hadi Stendi Mpya ya Bukoba Mjini (km 1.2) ambao utekelezaji wake unaendelea.
Dkt. Nchimbi ametoa maelekezo hayo mkoani Kagera, wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Bukoba Mjini.

“Nitumie nafasi hii kumtumia salamu Waziri wa Fedha huko huko alipo kwa uzito wake, Dkt. Mwigulu hawezi kushindwa kutafuta Bilioni 1.8 kwa muda mfupi, Kwahivyo naielekeza Wizara ya Fedha kutafuta hizi fedha haraka sana kwa ajili ya fidia za wananchi wa Bukoba Mjini”, Dkt. Nchimbi.
Awali, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, ameeleza kuwa Serikali inaendelea na upanuzi wa barabara njia nne kuanzia Rwamishenye mzunguko hadi Stendi Mpya ya Bukoba Mjini ambapo ujenzi huo ukikamilika itaendelea na Awamu ya Pili kuanzia Rwamishenye hadi Stendi Mpya ya Kyakailabwa na Awamu ya Tatu kuanzia Stendi ya Mpya ya Bukoba Mjini hadi Bandari ya Bukoba (Customs).
