
Katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayotarajiwa kufanyika tarehe 8 Machi, Wanawake wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) wameonyesha utashi wao wa kutambua na kuwahamasisha wanawake waraibu walioko katika nyumba za urekebishaji wa uraibu wa dawa za kulevya nchini.
Akizungumza na wanawake hao waliopata nafuu, Daktari wa DCEA, Dr. Joyce Kileju, amesema mamlaka hiyo inatambua mchango wa wanawake katika jamii na kwamba serikali inafanya jitihada mbalimbali ili kuzuia jamii kuingia kwenye matatizo ya dawa za kulevya.
"Tatizo la dawa za kulevya linazidi kusumbua jamii yetu. Leo hapa tumekuja kwa msingi mmoja: kinga na tiba. Njia mojawapo ya kutibu ni Soba House, ambayo inasaidia hasa wale wanaotumia pombe na bangi – dawa zinazopatikana kirahisi," amesema Dr. Kileju.
Ameongeza kuwa tangu kuanzishwa kwa DCEA, jumla ya nyumba 77 za upataji nafuu zimeanzishwa, na makao makuu ya mamlaka hiyo yamepanuka hadi mikoa mbalimbali ikiwemo Mwanza, Mtwara, Mbeya, Dodoma, Arusha na Tabora.
"Tunajitahidi kuhakikisha jamii inakomboleka kutoka katika tatizo la dawa za kulevya," amesema.
Dr. Kileju pia alieleza changamoto maalumu zinazokabili wanawake, ikiwemo unyanyapaa unaowakumba zaidi wanawake kuliko wanaume. Alisisitiza kuwa wanawake wanaweza kupatwa na madhara ya kiafya na kijamii kutokana na uraibu, ikiwemo kuharibika kwa mimba, matatizo ya hedhi, na unyanyasaji wa kijinsia.
"Mungu ametuumba wanawake kama kiwanda – tunabeba mimba, tunapambana na maisha. Lakini kupitia tiba za kisaikolojia na Soba House, wanawake wanapata nafuu na kurudi katika jamii," amesema.
Bridget Dyegula, Meneja wa Muungano Recovery Community (MRC), alishukuru DCEA kwa jitihada zao. Amesema uwepo wa wanawake hao unawapa motisha wale waliokata tamaa, na kuwaona kuwa inawezekana kupona na kurudi katika jamii.
"Mwanamke kupata nafuu ni changamoto, lakini akishikwa na mwanamke mwingine, anaweza kupata matumaini na nguvu ya kuendelea," amesema Dyegula.
Wengine waliopata nafuu, kama Zakia Zuberi, wamesema kupitia programu hizi wamepata matumaini mapya, mwamko wa kiroho na nafasi nyingine ya kujirekebisha, licha ya changamoto walizopitia kwenye jamii.
Aidha, Bokhe William kutoka Pili Missana Foundation alisisitiza umuhimu wa kuwezesha wanawake waliopata nafuu kujihusisha na shughuli za ujasiriamali, ili kuepuka kurudi katika tabia zao za awali za uraibu.
Kaulimbiu ya mwaka huu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani inasisitiza “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi Kufikia Dira 2050”, na DCEA imeahidi kuendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha wanawake waraibu wanapata msaada unaohitaji na kurudi kuwa sehemu ya jamii yenye afya na nguvu.
