Back to top

DKT. NOEL LWOGA APEWA TUZO YA UONGOZI BORA 2022.

28 November 2022
Share

Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt. Noel Lwoga ni miongoni mwa wakurugenzi bora 100 Tanzania kwa mwaka 2022 ambao walipewa tuzo zao Jijini Dar es Salaam.

Ushindi huo ni kulingana na uchambuzi uliofanywa na Kampuni ya Easternstar kwa kushirikiana na Taasisi ya Mameneja Tanzania (Tanzania Institute of Managers) na kampuni nguli ya kimataifa ya uchambuzi ya KPMG.

Aidha, Dkt. Noel Lwoga amekuwa mshindi wa tatu katika kundi la viongozi wa taasisi na mashirika ya Serikali sita zilizoingizwa kwenye kinyang’anyiro hicho.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo amewashukuru waandaaji na waratibu wa zoezi hilo kwa kumpendekeza kuwa sehemu ya washindi. Aidha, amesema tuzo hiyo ni kazi na juhudi kubwa inayofanywa na timu ya viongozi na wafanyakazi wa Makumbusho ya Taifa kwa ujumla.

Mgeni rasmi katika ghafla ya utoaji tuzo hizo, Mhe. Omary Shabani, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Zanzibar, aliwapongeza washindi wote na kuwataka waendelee kufanyakazi kwa weledi kwa manufaa ya taasisi zao na taifa kwa ujumla.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Mameneja Tanzania Deo Kilawe amesema kuwa taasisi yake ilianzisha kazi ya kutambua viongozi wanaofanya vizuri kwa sababu ya kujua kuwa uadilifu katika kazi ni jambo muhimu ambalo linatakiwa kufuatwa na kila mtumishi.

“Tulitafuta taasisi inayoaminika ili kuchambua wakurugenzi bora kwa mwaka 2022 bila kuleta malalamiko kwa jamii na KMPG wamefanyakazi hiyo kwa weledi mkubwa,” amesema Bw, Kilawe

Akizungumzia kuhusu tuzo hiyo Mkurugenzi wa Makumbusho ya Elimu Viumbe Jijini Arusha, Dkt. Christina Ngereza amesema, Dkt. Lwoga anastahili pongezi nyingi kwani kupitia uongozi wake shirikishi uliojaa upendo kwa watumishi anaowangoza umeifanya Taasisi ya Makumbusho ya Taifa iendelee kupiga hatua za kimaendeleo.

"Dkt Lwoga, hakika anastahili, ametujenga watumishi tumekuwa kitu kimoja, amepanua wigo wa mahusiano mema kati ya Makumbusho na wadau wa ndani na nje, anaheshimu kila mtumishi, sijawahi msikia anajivunia cheo chake wala kumnyanyasa mtumishi." Amesisitiza Dkt. Ngereza