Back to top

Dkt.Kijaji ataka tafiti zenye mikakati ya kukabiliana na Umasikini.

30 November 2019
Share


Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, amekitaka Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, kutafiti kwa kina namna wananchi wanavyoweza kuondokana na umasikini wa kipato pamoja namna Miradi mbalimbali ya Serikali inavyoweza kutekelezwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia thamani ya fedha kuliko ilivyo sasa.

Dkt.Kijaji ametoa rai hiyo wakati akiwatunuku astashahada na shahada mbalimbali wahitimu 3,182 Wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Kampasi ya Dodoma wakati wa sherehe za mahafali ya 33 ya chuo hicho.

Amesema kuwa matokeo ya tafiti hizo yataisaidia Serikali na Jamii kwa ujumla kupanga mikakati ya namna ya kukabiliana na umasikini wa wananchi hususani wa vijijini pamoja na kuharakisha maendeleo ya nchi kwa kuhakikisha kuwa miradi inayotekelezwa na Serikali inakuwa na tija.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango ambaye pia ni Kamishna Msaidizi wa Bajeti Bw. Pius Mponzi amemwahidi Dkt. Ashatu Kijaji, kwaniaba ya Baraza la Chuo hicho kwamba wataongeza jitihada katika eneo la utafiti na kuhakikisha kuwa matokeo ya utafiti huo yanawafikia wananchi kwa lugha rahisi.

Naye Mkuu wa Chuo hicho cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Profesa Hozen Mayaya amesema chuo chake kimetimiza miaka 40 tangu kianzishwe na kimepata mafanikio makubwa kwa kutoa wahitimu mahili na wenye kukidhi mahitaji ya soko.