Back to top

DKT.MABULA ATAHADHARISHA WANAOSUBIRI FIDIA NGARA

23 July 2023
Share

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula, amewatahadharisha wananchi wanaosubiri kulipwa fidia kupisha mradi wa uchimbaji madini wa Tembo Nickel wilayani Ngara mkoa wa Kagera kujiepusha na mikopo umiza.

Dkt.Mabula amesema hayo katika kijiji cha Bugarama wilayani Ngara, mara baada ya kutembelea mradi wa uchimbaji madini ya Tembo Nickel kwa lengo la kupata taarifa ya maendeleo ya ulipaji fidia kwa wananchi wanaopitiwa na mradi huo akiwa katika ziara yake ya siku moja wilayani humo mkoa wa Kagera.

Amesema, anawasikitia wale wananchi wote walioingia katika mikopo umiza kwa kueleza kuwa watalazimika kulipa kiasi kikubwa cha fedha na hivyo kutoona faida ya fidia ya mali zao.

"Hela yako yote umeshaikopa unakwenda kulipa pesa nyingi kwa pesa ndogo uliyoichukua mwisho wa siku unarudi katika umasikini bila sababu, niwaombe msikimbilie kukopa pesa unayokwenda kulipa ni asilimia kubwa ya kile ulichochukua"Amesema Dkt Mabula

Amesema, wanaowakopesha washajua muda mfupi ujao wananchi hao wanapata pesa hivyo wanajaribu kuwawahi watoe pesa leo lakini watakuja kulipa kiasi kikubwa cha fedha kuliko ilivyostahili jambo litakalowafanya kurejea kwenye umasikini.

Amewataka viongozi wa vijiji vyote vinavyopotiwa na mradi huo kutoa elimu ili wananchi wasije wakasikitika na kulia hapo baadaye kwa kuwa mara watakapopokea fedha za fidia basi waliowakopesha  watakuja kudai fedha zao.

Amewataka wananchi ambao hawajakopa kuacha kufanya hivyo kwa kuwa wanahitaji kuwa na maisha endelevu, kuwekeza ambapo alisema iwapo wanahitaji mikopo basi waende benki kwenye riba nafuu.

Awali Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alipata taarifa ya maendeleo ya ulipaji fidia wananchi wanaopisha mradi katika eneo la mradi.

Akiwa katika eneo hilo, Waziri Dkt Mabula alielezwa na kiongozi wa mahusiano ya jamii Bernard Sefu wa Kampuni ya Tembo Nickel kuwa, mgodi huo uko ndani ya kata tatu zenye vijiji vitano vinavyopisha mradi wa uchimbaji madini ya Nickel ambapo jumla ya wananchi 1,339 wanatarajiwa kulipwa fidia huku 349 kati ya hao wakijengewa nyumba kutokana na kuwa na makazi kwenye eneo la mradi huo.

Sefu alisema kuwa, mgodi huo umechukua hatua mbalimbali kwa kushirikisha viongozi, wataalamu na wananchi wanaopitiwa na mradi huo lengo likiwa kuhakikisha kila mwananchi anayehamishwa kupisha mradi anapata fidia stahiki kwa kufuata sheria za Tanzania na kanuni za kimataifa (IFC).

"Katika mchakato mzima wa kufanya ukokotovu wa malipo kwa wafidiwa, tuliwaonesha wahusika jedwali kabla ya kupeleka kwa mthamani mkuu wa serikali"Amesema Sefu

Kwa upande wake, Waziri Dkt. Mabula mbali na kuipongeza kampuni ya Tembo Nickel kuandaa utaratibu mzuri wa kulipa fidia wananchi wanaopisha mradi pamoja na kusaidia huduma mbalimbali za jamii. Hata hivyo, aliitaka kampuni hiyo kuhakikisha wale wananchi wanaoenda kujengewa nyumba na kampuni hiyo wanawekewa mpango wa makazi utakaokuwa katika mpangilio wa kimji.

"Wale wananchi mtakaowajengea nyumba muangalie namna ya kuwapanga, tunahitaji upangaji wa kimji walau ufanane na mahali pale, mkiweza kuwasaidia mtawafanya wafanane kimji"Amesema Dkt Mabula.

Kampuni ya Tembo Nickel Corporation Limited inatarajia kuchimba Madini ya Nickel katika eneo la Kabanga, Wilayani Ngara Mkoa wa Kagera ambapo zaidi ya hekta 4,000 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Januari 19 mwaka 2021 Serikali ya Tanzania na kampuni ya LIfezone Metals Nickel Limited zilisaini Mikataba uliowezesha kuanzishwa Kampuni ya Tembo Nickel Corporation Limited ambayo ni ya ubia kati yake na Serikali.