Back to top

EADB KUENDELEZA USHIRIKIANO WAKE NA TANZANIA

28 May 2024
Share

Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB), imeahidi kuendeleza ushirikiano uliopo kati yake na Tanzania kwa kuendelea kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo nchini. 

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha,  katika kikao kati ya Tanzania na Benki hiyo huko Nairobi nchini Kenya, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, alisema Tanzania ni mojawapo ya nchi zinazofaidika na uwepo wa Benki hiyo, kutokana na uhusiano mzuri uliopo kati ya pande hizo mbili.

Dkt.Mwamba alisema Benki hiyo imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali nchini ikiwemo miradi ya taasisi za Serikali kama vile Shirika la Nyumba, benki za biashara kama Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB) na miradi inayotokana na sekta binafsi.

Aidha Dkt.Mwamba alisema sanjari na ufadhili wa miradi ya EADB kwa Tanzania Bara, pia mazungumzo yanaendelea kuhusu miradi mingine kwa upande wa Zanzibar hasa miradi ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Zanzibar, Dkt.Juma Malik Akil, amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,  kupitia Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC) inatafuta ufadhili wa kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba takribani 3,000 za bei nafuu, hivyo Zanzibar inaona ni fursa kuitumia Benki hiyo kutekeleza mradi huo

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Bi. Viviene Yeda ametoa wito kwa Tanzania na nchi nyingine za Afrika Mashariki kuchangamkia fursa zinazopatikana katika Benki hiyo kutokana na uwiano uliopo katika umiliki wa hisa unatokana na Benki hiyo ambapo Tanzania, Kenya na Uganda zina hisa sawa.

Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) ni mshirika wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Standard Charter Bank ambayo inahudumia nchi wanachama sita (6) ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudani Kusini.