
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Mhe. Erasto Sima, amewataka watoa huduma za Fedha kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa na Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania wakati wa kutoa huduma za fedha kwa wananchi.
Agizo hilo amelitoa alipokutana na Timu ya wataalamu ya Wizara ya Fedha, ambao wamefika mkoani Kagera kwa ajili ya kutoa elimu ya huduma za fedha, kwa wananchi katika makundi mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara, wajasiriamali na wanafunzi.
“Watoa huduma ya fedha msifanye biashara kwa mazoea mfuate utaratibu uliowekwa na Serikali ukiwemo wa kupata leseni kwa mamlaka zinazotambulika kisheria kwa ajili ya kutoa huduma za fedha.”, alisema Mhe. Sima.
Kwa upande wake Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, alisema kuwa kutokana na wananchi wengi kutapeliwa wanapohitaji huduma za fedha, Wizara ya Fedha imeamua kutatua changamoto hiyo kwa kutoa elimu ya fedha kwa njia mbalimbali ikiwemo ya filamu.
Wizara ya Fedha imeanza kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali katika mikoa nane ikiwemo Kagera, Singida, Manyara ikiwa ni utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa mwaka 2021/2022 hadi 2029/2030.
