Back to top

FAO YAAHIDI KUENDELEZA SEKTA ZA MIFUGO, UVUVI.

10 September 2023
Share

Mkurugenzi Msaidizi na Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) upande wa Afrika, Bw. Abebe Haule-Gabriel amemuhakikishia Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega kuwa  Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza Sekta za Mifugo, Uvuvi na Kilimo hususan kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali katika sekta hizo hapa nchini. 

Bw. Abebe ametoa ahadi hiyo wakati wa mazungumzo baina yake na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega yaliyofanyika kando ya Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Barani Afrika (AGRF) jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

"Mhe. Waziri naomba kutumia fursa hii kukueleza kuwa FAO tumekuwa na ushirikiano mzuri na Tanzania na  tutaendelea kushirikiana katika kuendeleza sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kuendelea kuwainua wanawake na vijana wanaoshiriki katika sekta hizo", Amesema Abebe

Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega alilishukuru Shirika la FAO kwa ushirikiano wa kifedha na kitaalam wanaoutoa  katika miradi mbalimbali  inayolenga kusimamia na kuendeleza raslimali ya uvuvi hususani utekelezaji wa Mwongozo wa Hiari wa Uvuvi Mdogo (SSF Guidelines), Mpango Kabambe wa Sekta ya Uvuvi, na kuwawezesha wanawake katika sekta ya uvuvi huku akisema kuwa Serikali ipo tayari wakati wote kuendelea kushirikiana na Shirika hilo.